Thursday, March 9, 2017

Mfanyabiashara wa viroba ajiua Dodoma

Mfanyabiashara wa viroba ajiua Dodoma

Image result for kamanda wa polisi dodoma

KAMATAKAMATA ya wafanyabiashara wa viroba nchini, imesababisha kifo cha mfanyabiashara maarufu mjini hapa, Festo Mselia anayedaiwa kujiua kwa risasi baada ya kukaguliwa mara mbili na polisi kutokana na kumiliki bidhaa hiyo.

Kampeni ya kukamata wafanyabiashara wa viroba nchini, inayosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ilianza Machi mosi mwaka huu, baada ya Serikali kutoa taarifa ya mwisho wa biashara hiyo tangu Mei, mwaka jana.
Mei mwaka jana, Serikali ilibainisha kuwa kuanzia kipindi hicho hadi Januari mosi mwaka huu, ungekuwa mwisho wa kuzalisha na biashara ya pombe kali inayohifadhiwa katika vifungashio hivyo (viroba).
Hata hivyo, Januari Serikali iliongeza muda hadi Machi mosi ili kutoa nafasi tena kwa wafanyabiashara waliokuwa na shehena ya vinywaji hivyo waliofuata taratibu, kumaliza, lakini wengi wamekamatwa wakiwa nazo katika msako unaoendelea hivi sasa.
Mfanyabiashara huyo anayemiliki kampuni ya Mselia Enterprises na duka la bia za jumla, baa na nyumba za kulala wageni mjini Dodoma, alijipiga risasi kwenye shavu la kushoto juzi, Jumanne akiwa shambani kwake Veyula, nje kidogo ya mji wa Dodoma.
Daktari wa zamu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Carolyn Damian alisema alimpokea Mselia hospitalini hapo akiwa mahututi saa 7 usiku, na kumweka katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU) na robo saa baadaye alifariki.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Lazaro Mambosasa alithibitisha kupewa taarifa na mtu kuhusu kusikika kwa mlio wa risasi saa 3 usiku na baadaye saa 5 aliwatuma askari na kwenda kuchunguza na ndipo walipomwona mfanyabiashara huyo, amejipiga risasi na alikufa kutokana na kutokwa na damu nyingi.
Mambosasa alisema baada ya kupewa taarifa, askari walifuatilia eneo ambalo risasi zilisikika katika shamba la mfanyabiashara huyo eneo la Veyula na walipofika, waliokota maganda matano ya risasi alizotumia kujiua.
Mfanyakazi wa mfanyabiashara huyo, Leslie Msigwa alisema ni kweli polisi walikwenda mara mbili dukani kwake Barabara ya 11, karibu na Ofisi za TFDA, na mara ya mwisho waliondoka naye akiwa kwenye gari lake prado likiendeshwa na mteja wao, Mazengo hadi waliposikia kwamba amejiua shambani kwake, Veyula Dodoma.
Msigwa alisema ni kweli kwenye stoo yake, kulikuwa na katoni 1,269 za viroba pamoja na vinywaji vingine, ambavyo huwa wanasambaza katika baa na maduka mbalimbali.
Msigwa alisema Ijumaa iliyopita, polisi walifika dukani kwake wakiwa kwenye magari mawili wakiwa na silaha, wakaingia kukagua ndani na wakaondoka na wao, wakaenda benki kuweka fedha na kulipia mzigo iliyoagizwa.
Alisema walimtaka aripoti polisi Jumatatu ya wiki hii na alifanya hivyo na akarudishwa na polisi dukani na aliingia chumba cha kupumzikia, akalala hadi saa 1 usiku waliondoka kwenda nyumbani eneo la Area D.
Mfanyakazi huyo alisema juzi, aliitwa polisi, kila alipopigiwa simu alidai anakuja hadi ilipofika saa 10 ndipo zilikuja gari za polisi mbili pamoja naye, akashuka akaingia ndani na baadhi yao wakatoka na kuondoka, yeye aliwafuata akiwa kwenye prado ikiendeshwa na mteja wake, Mazengo.
Habari kutoka shambani kwake Veyula, zilisema ni kweli siku ya tukio, Mselia alikwenda na Mazengo, akamwacha nyuma mahali ilipo mifugo, yeye akaendelea mbele na walipoona anachelewa, walimfuata na wakaona amejeruhiwa kwenye shavu.
Msigwa alisema, yeye na mkewe walipoona anachelewa kurudi, walifunga duka na wakarudi nyumbani hadi ilipofika saa 2.30, wakaanza kupata taarifa kutoka kwa ndugu zao kwamba Mselia amejipiga risasi shambani Veyula.
Mtunza shamba, mtendaji, walonga
Mtunza shamba la Mselia aliyejitambulisha kwa jina la Baraka John, alisema wakati tukio linatokea yeye ndiyo alikuwa anatokea shambani, hivyo hakuona tukio lolote.
Alisema baada ya kufika nyumbani anakoishi, alimkuta Mazengo ambaye ni mtu wa makamo ambaye aliongozana na Mselia kwenda shambani. Alisema Mazengo alimwagiza achukue baiskeli, amfuate Mselia shambani kwani alimwambia amsubiri na amemsubiri kwa muda mrefu, hajarudi.
“Nilichukua baiskeli na kuelekea shambani kwa ajili ya kwenda kumwangalia, nilipofika shambani nilizunguka nikimtafuta bila mafanikio, nilianza kukata tamaa lakini nilipoangalia pembeni kwenye mti mkubwa nilimwona akiwa amelala chini, alikuwa akihangaika na damu nyingi zikimtoka, nikapata mshtuko na kugeuza baiskeli yangu na kwenda kumwambia mzee Mazengo pamoja na majirani. ‘’Mzee Mazengo alipiga simu polisi na wale majirani niliowaambia walitoa taarifa kwa diwani, mtendaji na mwenyekiti wa kijiji ambapo baada ya muda walifika na kuelekea eneo la tukio,” alisema.
John alisema baada ya muda, yalikuja magari mawili ya askari na kuelekea eneo la tukio, ambapo walimbeba majeruhi Mselia na kumpakina katika gari. Askari hao walifika nyumbani, wakaomba godoro ambapo niliwapa na kubeba majeruhi, lakini damu nyingi zilikuwa zikimtoka walielekea hospitali.
Akilizungumzia tukio hilo, Mtendaji wa Kata ya Msalato, Herman Malindila alisema alipigiwa simu saa 12 jioni kwamba kuna mtu amejipiga risasi katika eneo la mashamba. Malindila alisema baada ya kupokea taarifa hiyo, alifunga safari hadi eneo la tukio na kumkuta akiwa amelala chini huku pembeni kukiwa na bastola.
“Nilipofika eneo la tukio, niliukuta mwili wa mtu ukiwa umelala chini huku damu zikimtoka ilibidi tusubiri mpaka askari walipofika ndipo tukaanza kuubeba lakini damu zilikuwa zikimtoka kwa wingi,’’ alisema.
Huko Mpanda, Polisi wilayani humo mkoani Katavi imewakamata watu 16 wakiwemo wanawake watatu baada ya kukutwa na katoni 1,364 za pombe zinazofungwa katika vifungashio vya plastiki “viroba” vya thamani ya Sh 99,871,000.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda alisema jana kuwa wamekamata watuhumiwa hao na katoni hizo za viroba baada ya msako uliofanywa na Polisi kwa kushirikiana na wadau wa ulinzi na usalama, Mamlaka ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rukwa (Takukuru).
Alisema msako huo ulifanyika kwa siku mbili kuanzia Machi 6 hadi 7, mwaka huu katika maeneo mbalimbali katika Manispaa ya Mpanda ikiwemo kwenye maduka na baa.

No comments:

Post a Comment